| Mgomo wa madaktari wasambaa mikoani |
MGOMO wa madaktari ulioanza juzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), umesambaa na kuingia katika Hospitali za Mwanyamala na nyingine katika Mikoa ya Dodoma na Mbeya.Kutokana na hali hiyo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ametoa tamko akiwataka wawakilishi wa madaktari hao wafike ofisini kwake wakati wowote ili wazungumze naye na kupata suluhu ya tatizo hilo.Katika hospitali ya Muhimbili, mgomo huo jana uliingia katika siku ya pili huku madaktari wastaafu wanaofanya kazi kwa mkataba, wakipanga kuwasilisha pendekezo kwa uongozi wa hospitali hiyo kutaka kuwapunguzia kazi kwa kuondoa shughuli za upasuaji.
“Tunadhamiria kupeleka pendekezo kwenye uongozi wa hospitali hii ili kuwaeleza dhamira yetu ya kupunguza baadhi ya huduma zinazotolewa ikiwamo upasuaji. Hilo ni kutokana na madaktari wanaotakiwa kufanya kazi hiyo kuwa kwenye mgomo,” alisema mmoja wa madaktari hao ambaye hakutaka jina lake liandikwe.“Sisi katika idara hii tupo wawili tu, wagonjwa wanaokuja ni zaidi ya 150 tutawahudumiaje na wakati huohuo tunaitwa wodini? Alihoji daktari huyo.
Katika chumba cha wagonjwa wa dharura ambako juzi huduma ziliendelea, hali ilikuwa tofauti jana, kulikuwa na madaktari wawili tu ambao wameeleza kuwa wenzao wameingia kwenye mgomo. Ocean Road Mmoja wa wauguzi wa hospitali hiyo ambaye hakutaka kutajwa gazetini, alithibitisha wauguzi kutopokea wagonjwa wapya jana na kueleza kuwa ni kwa kuwa madaktari hawapo kazini.“Hatuwezi kuwapokea wagonjwa wakati watu wa kuwatibu hawapo. Hapa huduma zipo kwenye kitengo cha madaktari bingwa, mionzi na wagonjwa walioko wodini tu,” alisema. Mwananyamala Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk Kaliameli Wandwi hakutaka kuzungumza lolote kuhusu mgomo huo, alipobanwa alisema: “Sina muda wa kuongea na waandishi wenzako nimewakatalia tangu asubuhi.” Mbeya “Tungekuwa na uwezo kifedha tungekwenda katika hospitali za kulipia lakini sasa ni vigumu kwetu ambao hali zetu ni duni,” alisema Neema Emmanuel.Mgonjwa mwingine Winfrida Rashid alisema: “Hapa rufaa inaonekana kuna huduma zinaendelea kwa baadhi ya madaktari na manesi, lakini kasi imepungua, inawezekana wengine wakafanya kama kuigiza.” Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Mbeya, Dk Eleuter Samky alisema madaktari waliogoma ni 75, kati yao 10 wakiwa waajiriwa na 65 wanafunzi. Alisema hali ni mbaya kwa wagonjwa kutokana na kuwepo kwa mgomo huo na kwamba wanaofanya kazi ni wafamasia na madaktari bingwa na kitengo cha upasuaji na baadhi ya wauguzi katika kitengo cha mifupa. Dodoma “Ndugu yangu amelazwa tangu jana (juzi) asubuhi kwa ajili ya operesheni kubwa na hatakiwi kula chochote tangu hiyo jana (juzi) tukitegemea kuwa angefanyiwa operesheni leo,” alisema ndugu wa mgonjwa mmoja ambaye hakutaka kutajwa. Mwenyekiti wa Kamati ya kushughulikia madai ya watumishi wa Afya katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Dk Yahya Magaswa alisema wanaungana katika mgomo na madaktari wenzao nchini kote ili kuishinikiza Serikali kufanyia kazi madai yao ya msingi. “Tumemweleza Katibu wa Mkoa madai yetu ya msingi na sababu za kuungana na wenzetu katika mgomo ulioanza kote nchini... ameahidi kuyafanyia kazi na sisi tumekubaliana kutoa huduma za dharura tu mpaka kesho jioni tutakapokutana tena kujadili majibu yatakayotolewa na Serikali,” alisema Magaswa. “Kupitia kwenu vyombo vya habari, naomba mfikishe ujumbe huu kwamba niko tayari kufanya mazungumzo na madaktari hao. Sijali kama ni uongozi gani jambo la msingi uwe unawakilisha madaktari,” alisema. Alisema akikutana na madaktari hao, atawabembeleza wasitishe mgomo na kuendelea kutibu wagonjwa huku, wao na Serikali wakiendelea na mazungumzo ya kudai maslahi yao. Alisema kimsingi, madaktari hao ambao wako kwenye mafunzo ya vitendo walikuwa na madai ya msingi baada ya kukosa posho zao za Novemba na Desemba, lakini jambo hilo halifungi mlango wa mazungumzo. Pinda alisema kinachofanyika kwa madaktari hao ni kulipwa posho ambazo si mshahara hivyo, fedha zake zinatoka katika matumizi ya kawida (OC), ambayo wakati mwingine huchelewa. Kwingine shwari “Mimi si msemaji wa mkoa lakini kwa vile ni kiongozi wa ulinzi na usalama nakuthibitishia hakuna mgomo ingawaje kuna watu pengine walipenda uwepo lakini leo hakuna,” alisema Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Henry Clemence. Katika hospitali ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure, madaktari waliendelea na kazi. Mmoja wa madaktari waliokuwa kazini, Dk Denis Kashaija alisema wanaendelea kuchapa kazi za kutoa huduma kwa wagonjwa.“Kama unavyoshuhudia, sisi na wauguzi hatujagoma kutoa huduma kwa wagonjwa tunaendelea na kazi labda itokee kuanzia kesho,” alisema Dk Kashaija. ( Source: Mwananchi)
|
MGOMO wa madaktari ulioanza juzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), umesambaa na kuingia katika Hospitali za Mwanyamala na nyingine katika Mikoa ya Dodoma na Mbeya.Kutokana na hali hiyo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ametoa tamko akiwataka wawakilishi wa madaktari hao wafike ofisini kwake wakati wowote ili wazungumze naye na kupata suluhu ya tatizo hilo.Katika hospitali ya Muhimbili, mgomo huo jana uliingia katika siku ya pili huku madaktari wastaafu wanaofanya kazi kwa mkataba, wakipanga kuwasilisha pendekezo kwa uongozi wa hospitali hiyo kutaka kuwapunguzia kazi kwa kuondoa shughuli za upasuaji. 










