| UJASIRI WA UFISADI |
|
Kifungu hicho cha Mkataba kilikuwa kinaruhusu mkataba huo uliokuwa na thamani ya dola milioni 172.5 kuahulishwa kwenda kwenye kampuni nyingine baada ya makubaliano ya pande hizo mbili tena kwa maandishi. Sehemu ya kifungu hicho cha mkataba huo ambao FP inao kinasema wazi kuwa “Neither party may assign this agreement or grant any security interest, charge, lien, or other encumbrance in this Agreement other than by mutual agreement between the parties in writing”. Kwa maneno mengine, mkataba ulikataza pande zote mbili (TANESCO na RDC) kuhaulisha jukumu lolote au jambo lolote linalohusiana na mkataba huo kwenda kwa kampuni au chombo kingine pasipo makubaliano ya maandishi kati ya pande hizo mbili. Hivyo kitendo chochote kwa upande wa TANESCO au Richmond kuhamisha mkataba au majukumu yake kwenda kwa chombo kingine bila ridhaa ya kimaandishi ya mwenzake ilikuwa ni uvunjaji wa mkataba huo. Hata hivyo, katika taarifa ambazo Kamati Teule iliyoundwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuchunguza Richmond ilipatiwa chini ya kiapo kampuni ya Richmond ilihamisha mkataba wake kwa Dowans Holding S.A tarehe 23 Disemba, 2006.
Mlolongo wa matukio kwa mujibu wa ripoti ya Kamati teule hadi kufikia RDC kuhamisha unaonesha kuwa Shirika la Ugavi wa Umeme la Tanzania lilifichwa ukweli wa kilichokuwa kinaendelea kwani haikujua kuwa wakati wote inafikiria ugumu wa kuhamisha mkataba huo kwenda Dowans kampuni ya Richmond tayari ilikuwa imeshauhamisha mkataba huo. Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyosomwa kwa kile kilichodaiwa na aliyekuwa Waziri Mkuu Bw. Edward Lowassa kuwa ni “kwa mbwembe” inaonesha kuwa TANESCO waliandikia RDC barua tarehe 27 Oktoba, 2006 ya tahadhari kuwa RDC ilikuwa inaonesha kushindwa kutekeleza masharti ya mkataba (default notice) iliyotaka majibu kufuatia mapungufu kadhaa ambayo TANESCO waliyaona. Ripoti hiyo inasema kuwa kwa mujibu wa TANESCO mapungufu hayo yalikuwa ni pamoja na “kushindwa kwa kampuni hiyo kusafirisha angalau mtambo wa kwanza wa wastani wa unit 22 kW kuja Tanzania; kushindwa kwa kampuni hiyo kutoa taarifa za mara kwa mara za maendeleo ya utekelezaji wa mradi; uwepo wa kampuni hiyo Marekani kihalali; uwezo wa kampuni hiyo kitaalamu na kifedha kuweza kutekeleza Mkataba huo wa umeme wa dharura katika muda muafaka.” Lengo la taarifa hiyo ilikuwa ni kutaka majibu kutoka RDC ya kwanini TANESCO isione kuwa Richmond wameshindwa kazi na hivyo kuvunja mkataba. Barua hiyo ya tahadhari haikujibiwa. Kwa mujibu wa Ripoti ya Mwakyembe shirika la TANESCO likaandika barua nyingine za tarehe 17 na 23 Novemba, 2006 “kuikumbusha (Richmond) kuhusu hoja zake za awali (za barua ya Oktoba 27, 2006) ambazo hazikujibiwa na kudai maelezo kuhusu taarifa za kwamba kampuni hiyo haikuwa na mahusiano na Pratt & Whitney iliyotegemewa sana kubeba sehemu kubwa ya majukumu ya mradi.” Hata hivyo barua zote hizo tatu hazikujibiwa wala hoja zilizoibuliwa na TANESCO kupewa majibu yenye ushawishi wa ukweli na mvuto wa kiakili. Na siku hiyo ya Novemba 23, 2006 Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO alijieleza kwa Waziri juu ya tatizo lililokuwa linaonekana kuhusu uwezo wa Richmond. Tarehe 28 Novemba, 2006 yaani siku tano baada ya barua ya Mkurugenzi wa TANESCO Waziri wa Nishati Bw. Nazir Karamagi alimpigia simu aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO Balozi Fulgence Kazaura kumtaarifu kuwa kampuni ya Richmond ilikuwa inakusudia kuhaulisha mkataba wake kwenda kampuni “nyingine” na hivyo alitaka kujua kama mkataba uliruhusu uwezekano huo. Ripoti ya Mwakyembe inasema kuwa “Tarehe hiyo hiyo 28 Novemba 2006 uongozi wa TANESCO ulimshauri Mwenyekiti wa Bodi kama ifuatavyo:- (i) Mkataba kati ya Richmond Development Company LLC na TANESCO hauruhusu kukabidhi majukumu ya Mkataba kwa Kampuni nyingine isipokuwa kwa maafikiano ya pande mbili za Mkataba (Kifungu 15.12).” Tarehe 4 Disemba, 2006 (chini ya siku kumi tangu Karamagi adokeze nia ya Richmond kuhamisha mkataba) TANESCO walipokea barua kutoka Richmond ambayo ilionesha kuwa kampuni hiyo ilitaka “kutumia haki yake chini ya Kifungu 15.12 cha Mkataba ili kuhamisha majukumu yake yote ndani ya Mkataba huo kwenda kwa DOWANS Holdings, S.A. Aidha, Richmond Development Company LLC ilieleza kwamba tarehe ambayo TANESCO itaridhia mapendekezo hayo iwe ndiyo tarehe rasmi ya kuhamisha mafao na majukumu yote kwa DOWANS Holdings, S.A na kwamba DOWANS Holdings, S.A itawasilisha vielelezo vya utambulisho wake kwa TANESCO” Hata hivyo, barua hiyo ambayo TANESCO waliipokea Disemba 4, inaonesha kuwa iliandikwa Novemba 9, karibu mwezi mmoja kabla. Siku moja kabla ya kupokea barua ya Dowans kutaka kuhamishia mkataba wake kwa Dowans yaani tarehe 8 Disemba, 2009 TANESCO ilikuwa imeiandikia Benki ya Citibank isaidie kufanya uchunguzi wa kujua kampuni ambayo Richmond ilikuwa inataka kuhamishia mkataba wake ilikuwa ni kampuni gani na yenye uwezo gani kwani “la “kwani japokuwa masharti ya Mkataba yanaruhusu Mkataba kuhamishwa, TANESCO ingependa kufahamu hasa ni nani anayehamishiwa Mkataba huo” Kamati Teule haikufanikiwa kupata majibu ya Citibank ila iliambiwa kulikuwa na shinikizo toka Wizarani “kuwa viongozi wa Wizara kama kawaida yao waliishinikiza TANESCO kukubaliana na ombi la Richmond Development Company LLC la kuhamisha mkataba.” Ni kutokana na hilo tarehe 21 Disemba, 2006 TANESCO ikaiandikia kampuni ya Richmond kukubali uhaulishaji wa mkataba huo kwenda kwa Dowans kwa barua yenye SEC. 388/12/206 ambapo pamoja na mambo mengine ilitaka “ipate hati ya uthibitisho kutoka Dowans Holdings, S.A ya kuridhia uwajibikaji kamilifu katika kutekeleza Mkataba wa tarehe 23 Juni, 2006, kati ya TANESCO na Richmond Development Company LLC.” Hivyo tarehe 23 Disemba 2006 Mkataba ukaingiwa kati ya TANESCO na Dowans S.A ambao ulikuwa ni kuhamishia mkataba kati ya TANESCO na Richmond kwenda kwa Dowans Holdings S.A. Kwa mujibu wa ripoti ya Kamati Teule kusainiwa kwa mkataba huo kati ya TANESCO na Dowans Holding S.A kulileta mambo matatu muhimu ; kwanza, “Tarehe 23 Disemba 2006 ndiyo siku rasmi ambayo Richmond Development Company LLC imekabidhi rasmi majukumu yake ya utekelezaji wa Mkataba kati yake na TANESCO kwa Dowans Holdings S.A”; Pili, “Dowans Holdings, S.A itatekeleza majukumu ya Mkataba uliotiwa saini kati ya TANESCO na Richmond Development Company tarehe 23 Juni, 2006 kwa masharti yote kama yalivyo katika Mkataba”; na tatu, “Malipo halisi na madeni ndani ya Mkataba kati ya TANESCO na Richmond Development Company LLC, sasa yatakwenda kwa Dowans Holdings, S.A kuanzia tarehe 23 Disemba, 2006.” Hata hivyo kulikuwa na tatizo; Richmond Development Corporation LTD ilikuwa tayari imeshahamisha mkataba wake na TANESCO kwenda kwa Dowans miezi karibu miwili nyuma. Yaani, RDC iliingia mkataba na Dowans Holdings S.A tarehe 14 Oktoba, 2006 bila ya kushirikisha, kutaarifu au kwa namna yoyote ile kupata maridhiano ya kimaandishi toka kwa TANESCO kinyume cha kipengele cha 15.12 tulichokiona hapo juu. Hii ina maana kuwa mazungumzo yote yaliyofuatia hadi TANESCO kukubali kuwa Richmond ihamishe mkataba kwenda kwa Dowans SA katika barua ya Disemba 21, 2006 yalikuwa ni kanyaboya, au danganya toto kwani wakati TANESCO inaingia ikiamini (in good faith) kuwa Richmond ilikuwa bado haijahaulisha mkataba kwa Dowans, Dowans iliingia ikijua kuwa tayari imekwisha fanya hivyo. Kampuni ya Richmond ilihamisha mkataba wake kwenda Dowans tarehe 14 Oktoba, 2006 ikikabidhi majukumu yake yote iliyokuwa imekubaliana na TANESCO kwenda kwenye kampuni hiyo inayodaiwa kuwa ni ya Costa Rica. Mkataba huo uliingiwa kabla tu ya mitambo ya kwanza kusafirishwa kwa ndege kupelekwa Tanzania. Siku hiyo hiyo wakati Richmond inahamisha mkataba wake wa Juni 23, 2006 na TANESCO kwenda Dowans Holdings S.A ilihamisha vile vile mkataba wake wa Septemba 25, 2006 kati yake na Vulcan (Vulcan Advanced Mobile Powers Systems, LLC na Vulcan Power Group, LLC) wa ununuzi wa mitambo toka kampuni hiyo kwenda kampuni ya Dowans Holdings S.A. Ni muhimu kutaja kuhamishwa kwa mkataba wa Richmond na Vulcan kwenda Dowans S.A kwa sababu mara baada ya mkataba huo kuhamishwa kwa Dowans S.A kampuni hiyo ililipa Vulcan dola milioni 7.5 na ikanunua mtambo wa kwanza wa gesi ambao uliingizwa nchini mwishoni mwa 2006 na kupokelewa kwa shangwe. Wakati baadhi ya magazeti yaliripoti kuwa “mitamo ya Richmond yawasili” ukweli ni kuwa mitambo hiyo ilikuwa ni ya kampuni ya Dowans Holdings S.A ambayo ndiyo ilinunua na kugharimia kuingizwa kwake nchini. Hili hata hivyo linaleta matatizo makubwa mawili ya kisheria ambayo yote yanahusiana na malipo ya shilingi bilioni 94 ambayo kampuni ya Dowans S.A inatarajiwa kulipwa siku chache zijazo kufuatia hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (International Court of Arbitration). Tatizo la kwanza ni kuwa wakati aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Bw. Nazir Karamagi alipozungumza na aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO Balozi Fulgence Kazaura Novemba 28, 2006 kuulizia kama mkataba wa Richmond unaruhusu kuhamishwa kwenda kampuni nyingine, kampuni ya Richmond ilikuwa tayari imekwisha hamisha mkataba huo kisheria kwenda Dowans Holdings S.A. Hii ina maana kuwa yote yaliyofuatia hapo hadi baadaye TANESCO kukubali kuhamisha mkataba kwenda Dowans kwa barua yake ya Disemba 21, 2006 yalikuwa ni mazingaombwe tu ya kujaribu kutimiza matakwa ya kifungu cha 15.12 cha mkataba wa Richmond na TANESCO kama tulivyoona hapo juu. Ilikuwa ni muhimu kwa Richmond kutimiza kifungu hicho kwa sababu vinginevyo mkataba kati yake ya Dowans usingekuwa halali kwani ungekuwa umehaulishwa kinyume cha makubaliano. Hili linatuleta kwenye kuelewa kwanini jitihada zote za TANESCO kuitaarifu Richmond kuwa ilikuwa inaelekewa kushindwa kutekeleza mkataba hazikuzaa matunda. Inafafanua kuwa kwanini barua za Oktoba 27, Novemba 17, 23 na 29 kwenda kwa Richmond hazikujibiwa na badala yake maelekezo ya Waziri Karamagi (Novemba 28, 2006) kwa Kazaura kuwa “Richmond Development Company LLC walikuwa wanataka kuhamisha majukumu yao yaliyobaki katika Mkataba wa uletaji mitambo na uzalishaji umeme wa dharura kwa kampuni nyingine.” Majibu yaliyotolewa siku ile ile kwenda kwa Waziri kuwa “ Kifungu cha 15.12 cha Mkataba huo hakiruhusu kukabidhi majukumu ya Mkataba kwa Kampuni nyingine isipokuwa kwa maafikiano ya pande mbili za Mkataba.” Hili lilithibitisha tatizo ambalo Richmond waliligundua baada ya kuingia mkataba na Dowans Oktoba 14, 2006 bila kuwashirikisha TANESCO. Hivyo, mpango wa “kuwashirikisha TANESCO” ukaingizwa na hatimaye TANESCO wakakubali na “mkataba” ukahamishwa “rasmi” kwenda Dowans Disemba 23, 2006 kama Ripoti ya Mwakyembe ilivyoonesha. Hii ina maana Richmond ilivunja mkataba na TANESCO pale ilipoamua kuhamisha mkataba wake huo kwenda kwa Dowans Oktoba 14, 2006 bila ya ridhaa, ushauri, makubaliano ya kimaandishi kati yake na TANESCO kama kipengele cha 15.12 cha Mkataba kilivyotaka. Richmond ilijua kuwa imefungwa na kipengele kingine ambacho kiliweka wazi kuwa endapo ingehamisha mkataba huo bila ya kuihusisha TANESCO basi itakuwa imejiingiza matatani. Kipengele hicho ni cha 12.1e ambacho ni sehemu ya mambo ambayo yatafanya Richmond kuwa imeelekea kushindwa kutekeleza mkataba. Hivyo, Richmond ilikuwa haina jinsi nyingine kwa sababu isingeweza kuiambia TANESCO kuwa tayari imeingia mkataba na Dowans kwani itakuwa ni sababu tosha kwa TANESCO kuvunja na isingeweza kuvunja tena na mkataba na Dowans S.A kwani tayari Dowans walishaingia gharama za kununua majenereta toka Vulcan. Njia rahisi ilikuwa kuanzisha mazingaombwe ya “kuhaulisha mkataba kwenda kampuni nyingine”. Hili hata hivyo linatuingiza kwenye tatizo kubwa la pili ambalo linahusiana moja kwa moja na malipo ya Bilioni 94 kwenda Dowans S.A siku chache zijazo. Kesi iliyoamuriwa na ICC-ICA ilizingatia kati ya mambo mengi uhalisia na uhalali wa mkataba wa Dowans. Sehemu kubwa ya hukumu hiyo ilishughulikia ukweli kuwa mkataba uliokuwa umeingiwa na TANESCO na Dowans wa Disemba 23, 2006 ulikuwa ni halali. Katika hukumu hiyo kilichoangaliwa ni makubaliano ya kuhamisha mkataba kutoka kwa Richmond kwenda Dowans Holdings S.A kama yalivyoanzishwa na mawasiliano ya simu kati ya Waziri Nazir Karamagi (akiwa Calgary, Canada) kwenda kwa aliyekuwa mwenyekiti wa bodi Balozi Kazaura Novemba 28, 2006. Kuna mambo ambayo tuna uhakika nayo na ambayo ni msingi wa hatimaye kukataa kuwalipa Dowans S.A na Dowans Tanzania Limited tuzo iliyotolewa na Mahakama ya Usuluhishi wa Kibiashara (ICC). Mambo yafuatayo ni ya kuzingatia. 1.Wakati Karamagi anawasiliana na Kazaura kuulizia kama mkataba wa Richmond/TANESCO unaruhusu kuhamishika alikuwa tayari na taarifa kuwa Richmond walikuwa tayari wameshahamisha mkataba kwenda Dowans, SA Oktoba 14,2006 (mwezi mmoja na nusu kabla) Hukumu hiyo ikadai katika kifungu cha 519 kuwa “based on the evidence adduced before the Tribunal these representations presented in the dossier of 8 December 2006 were statements of fact, were true”. Yaani, “ kulingana na ushahidi uliotolewa katika mahakama yaliyosemwa katika barua ya Disemba 8, 2006 yalikuwa ni madai ya uhakika, yalikuwa kweli”. Ni kutokana na msimamo huo wa mahakama hiyo hoja kuwa Dowans haikuwa mkweli wakati inataka kuchukua mkataba wa Richmond ilitupiliwa mbali katika kifungu cha 524. Baada ya kutupilia mbali hoja hiyo kwa makosa mahakama hiyo ikaangalia kile ilichoamininishwa kuwa ndio makubaliano ya kuhamisha mkataba toka Richmond kwenda Dowans. Katika kifungu cha 533 cha hukumu hiyo inaoneshwa kuwa kulikuwa na makubaliano ya kuhamishia mkataba kati ya TANESCO na Richmond kwenda Dowans kwa barua iliyoandikwa Disemba 21, 2006 (kama tulivyoona hapo juu). Na hili lilikuwa kweli kwani ni tarehe 23 Disemba, 2006 mkataba huo ukapelekwa kwa Dowans. Na hata uamuzi wa baadaye wa TANESCO kukubali mkataba uhamishiwe toka Dowans S.A kwenda Dowans Tanzania Limited ulitegemea uhalali wa kitendo cha Disemba 21 na 23, 2006. 1.Kama Richmond ilikuwa tayari imeshahamisha mkataba wake na TANESCO kwenda Dowans S.A Oktoba 14, 2006 ni kitu gani kilikuwa kinafanyika kwa majadiliano ya kuanzia Novemba 9 hadi TANESCO kukubali kuhamishwa mkataba Disemba 21, 2006? Kutokana na uzito wa ushahidi ambao tumeupendekeza mbele ya wasomaji na Watanzania wenzetu tunajikuta tunabakia na mapendekezo yafuatayo tu: 1.Serikali isilipe hata senti moja na iamue kujitoa kwenye Mahakama ya Usuluhishi na badala yake Bunge letu liimarishe sheria zetu za usuluhishi wa kibiashara ili mikataba yote inayohusiana na umma inapotokea matatizo iamuliwe kwa sheria zetu wenyewe. SWALI PEKEE AMBALO LINAWEZA KUVUNJA HOJA HII WAULIZWE DOWANS S.A na watetezi wa malipo haya haramu ni hili - Ni lini Dowans Holdings S.A. walirithishwa mkataba wa Richmond/Tanesco?
Radio Mbao imeona ni jukumu lake kuweka mwanga kwa habari za kuielewesha jamii. Hii habari sio ya Radio mbao, imenukuliwa kutoka kwa Jamii Forum. Unaweza toa maoni yako hapo chini. Source: Habari hii inamilikiwa na JamiiForums.com
|
Mkataba kati ya TANESCO na Richmond Development wa tarehe 23 Juni, 2006 wa kuingiza majenereta ya umeme kufuatia upungufu wa nishati hiyo uliokuwa umekithiri nchini mwaka 2006 ulihamishiwa kwa kampuni ya Dowans Holdings S.A tarehe 14 Oktoba, 2006 mwezi mmoja kabla bila ya kuihusisha TANESCO kama ilivyotakiwa kwa mujibu wa kifungu 15.12 cha mkataba huo.










